Uncategorized

Kwa nini Jamii Yetu

Mwandishi: Robert Matovu

Baada ya kuchapisha Makala yangu ya kwanza kwenye blog hii, rafiki yangu wa siku nyingi, kuanzia utotoni aliniuliza ni kwa nini nilichagua jina “Jamii Yetu”.  Alitaka kujua pia ni kwa nini nianze na makala inayoangazia uhusiano wa Rwanda na Uganda.

Majibu kwa maswali yake mawili hayakuwa rahisi kutolewa kwa ufupi. Imebidi nimpe historia fupi ya huzuni niliyo nayo kama mzalendo wa Uganda kutokana na kuzidi kwa uhasama wa serikali ya Uganda dhidi ya raia Rwanda.

Mwaka 1973, wazazi wangu alikimbilia Tanzania kutokana na utawala wa Idd Amin Dada. Wakati huo nilikuwa na umri wa miaka sita (6).  Nililazimika kuanza shule ya msingi Jijini Dar es Salaam, tulipokuwa tukiishi. Ni katika maisha hayo nilipojikuta naishi maisha katika ,jamii nyingine iliyonijali baada ya kushindwa kuishi katika nchi yangu.

Kati ya majirani zetu Dar es salaam, ilikuwa ni familia ya Mnyarwanda aliyekuwa mkimbizi nchini humo kwa miaka kadhaa. Wazazi wangu walikuwa marafiki wa familia hiyo ya bwana Joseph (nalikumbuka jina lake moja tu) aliyekuwa na watoto wawili mkubwa akiwa ni wa umri wangu. Nileelezwa na wazazi wangu pia, kuwa urafiki wao ulitokana na mshikamano wa kuwa wote ni wakimbizi.

Mara nyingi baba au mama walimtembelea Joseph na mkewe ambaye simkumbuki jina. Kadhalika familia hiyo ilikuja kwetu kwa mazungumzo ya kawaida. Wakati mwingine wakati wa mazungumzo yao, walikuwa wanatufukuza tusifuatilie ni nini kinachozungumzwa.

Katika maisha yetu hayo, nakumbuka nikiwa darasa la nne, tulipata ugeni wa mtu ambaye baba alininong’oneza kuwa ni rafiki yake anayeitwa Yoweri Museveni ambaye ni mkimbizi kutoka Uganda, lakini aliyekuwa anakaa mjini Moshi kaskazini mwa Tanzania.

Mwaka 1980, nikiwa darasa la tano, baba alituaga akarudi Uganda. Alituacha Tanzania na mama kwa sababu ya masomo. Baadaye sana, nikiwa naingia ujanani, mama alitueleza kuwa ilikuwa si busara kuipeleka familia yote Uganda kwa sababu za kiusalama na kiuchumi.

Na kweli ilikuwa hivyo, kwa vile mama na baba walikuwa na kazi Tanzania na isingekuwa vizuri kuishi katika maisha mengine ya mashaka bila mpango. Mwaka 1982, familia ya jirani yetu Uncle Joseph kama nilivyokuwa namuita, ilipokea familia zingine mbili za wanyarwanda ambao hawakuwa wametoka Rwanda bali Uganda.

Familia hizo mbili za watu tisa, walikuwa wakimbizi. Kutokana na msongamano kwa uncle Joseph, familia moja ilihamia kwetu kwa kuwa wakubwa zangu wote walikuwa wanasoma Kenya walikokuwa wakikaa na Uncle yangu George Kibuuka.

Mwezi Juni mwaka 1986, familia yetu na zile mbili zilizokimbilia Tanzania mwaka 1982, tulirudi Uganda. Nakumbuka siku mama aliponiambia kuwa yule Rafiki yao Museveni ndiye Rais wa Uganda.

Baada ya kurudi Uganda nilipewa maelezo yaliyonisaidia kujua ni kwa nini kuna wanyarwanda walilazimika kukimbilia Tanzania. Waliukimbia utawala wa Milton Obote aliyekuwa anawanyanyasa na kuwaua akiwashutumu kuwa ndio walikuwa ni uti wa mgongo wa waasi wa National Resistance Army (NRA). Maelfu kwa maelfu kati yao walifukuzwa wakatupwa Rwanda, na utawala wa Rais Juvenal Habyarimana ukawakataa.

Kurudi kwetu Uganda kulinifanya nitambue kuwa uwe Mganda, uwe Mtanzania, au Mnyarwanda ni familia moja tu ya Afrika ya mashariki. Tulifika nchini kwetu nikiwa kijana mwenye ufahamu wa kutosha. Niliambiwa na wazazi wangu, familia yetu kuhusu mchango wa Wanyarwanda katika mapambano ya kumng’oa Amin na Obote na jinsi maelfu walivyojitoa mhanga wakamwaga damu yao kuikomboa Uganda, kama bima ya Usalama wa nchi iliyowapokea.

Nilikuwa na marafiki wengi kati yao, hasa nilipojiunga na jeshi la NRA mwaka 1987. Nidhamu waliyokuwa nayo, uzalendo na ushupavu wa vijana wa Kinyarwanda nilioishi nao, ulinifanya nijenge uhusiano nao wa kudumu.

Hakuna kitu kilichokuwa kinanisikitisha kama kuwasikia baadhi ya Waganda wenzangu wakilalamika kuwa kuna wanyarwanda wengi katika jeshi letu kana kwamba vita waliyoipigana kwa miaka zaidi ya saba ilikuwa ni lelemama. Mchango wao ungepashwa kuwa ni wa kusifiwa na siyo kulaaniwa.

Mwezi Oktoba 1990, wanyarwanda wakiongozwa na Meja Jemadari Fred Rwigyema, kwa hiari yao, waliachana na NRA wakaenda kupigana vita vya kuikomboa nchi yao ya Rwanda. Waliokuwa wanaudhiwa na kuwa na wanyarwanda kwenye jeshi letu, walifurahi. Mimi na wengine wengi tuliokuwa tunaheshimu mchango wao, tulisikitika lakini tukabaki tunawaombea wafanikiwe kwa kuwa ni jamii yetu.

Leo hii ninapoona Rais Yoweri Kaguta Museveni, mdogo wake Jemadari Salim Saleh, Jemadari Henry Tumukunde na Idara ya ujasusi wa kijeshi wa Uganda (CMI) wakiwaunga mkono kundi la magaidi wa Rwanda National Congress (RNC) nasononeka sana.  Ni usaliti mkubwa.

Nchi zetu hizi mbili zingepashwa kuwa na mshikamano madhubuti kutokana na historia ndefu tuliyo nayo. Ni jamii yetu. Rais Paul Kagame wa Rwanda, hayati Rwigyema na wenzao wengi waliojitolea kuitetea Uganda ni mashujaa wetu. Kuwachukulia kama maadui na mahasimu ni aibu kwa jamii na nchi yetu ya Uganda. Ikumbukwe, asiyeshukuru ni kaffir.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

%d bloggers like this: